top of page

ANGALAU –– INGAWA- INGAWAJE - ANGALI …

  • A. Ferrari (video KTN)
  • 23 avr. 2016
  • 2 min de lecture

Lazima kuwa makini kutochanganya viunganishi hivi ( angalau, ingawaje, angali, ingawa...) na kuvitumia vizuri.

1. Kiunganishi cha angalau au angalao (au angaa) kinatumika kueleza jambo lililo bora zaidi.

Kwa mfano :

a) Angalau kaa chini umechoka.

Maana : bora ukae chini, umechoka.

Angalau inaweza kutumika pia kusema kwamba ni bora kuliko hali ya sasa hivi lakini inaweka mkazo kuwa kuna suluhisho nyingine bora. (kwa Kiingereza at least)

b) Inawalazimu kuanza upya mchakato wa kutafuta katiba mpya au angalao kurejesha mjadala wa kitaifa kuhusu rasimu ya pili ya Warioba.

2. Viunganishi ingawa, au ingawaje vinatumika kama vile : hata, ijapokuwa au japo.

a) Kauli hiyo imenisikitisha sana ingawaje haikunishangaza.

b) Alisema kwamba ingawa ugaidi umekuwepo, Kenya bado ni nchi ya kuvutia.

3. Kiambishi awali ya kitenzi + ngali : kuwa bado

Ngali ikitumiwa kama kitenzi humaanisha” kuwa bado”.

Ngali hutumika katika Kiswahili bora na Kiswahili cha watu wa pwani, japo neno la bado hutumika sana na watu wa bara.

a) Hali yake imeboreka lakini ingali mahututi (hali yake imeboreka lakini yeye huwa bado mahututi)

b) Vita ya ubakaji ingali mbichi. (vita ya ubakaji huwa bado mbichi)

c) Anataka kujua jinsia ya mtoto angali mimba. (mtoto bado yupo tumboni mwa mama yake)

d) Binadamu huanza kujifunza mambo mbali mbali tangu alipokuwa angali mdogo. (alipokuwa bado mdogo)

e) Watu hawa wangali wanafanya kazi serikalini ingawa wameshtakiwa kufanya vitendo vya rushwa. (watu hawa ambao bado wanafanya kazi serikalini..)

f) Alipokuwa angali mchanga, walianza kumfundisha kazi ya ujenzi. ( Alipokuwa bado mchanga..)

Ngali pia hutumika na kiambishi –po kwa maana ya kuwapo bado mahali.

g) Mgomo wa walimu ungalipo. (mgomo wa walimu huwapo bado)

Ngali hutumiwa sana katika methali, kwa mfano:

h) Usitukane wakunga na uzazi ungalipo.

Maana: usitukane wakunga kama mjamzito anazaa sasa hivi/ kabla hajamaliza kazi (ya kuzaa).

NB : Pia ngali inaweza kuwa wakati. (past conditional kwa Kiingereza)

Kwa mfano : Ningaliwenda mapema sokoni, ningalipata mapapai.

Mazoezi: Tizama video hiyo kisha tunza sentensi tatu kuhusu mambo yanayozungumzwa katika video:

  • katika sentensi ya kwanza, tumia “ingawa/ingawaje”

  • katika sentensi ya pili, tumia angali au wangali.

  • katika sentensi ya tatu, tumia angalau au angalao.


Comentarios


  • Facebook Clean Grey
  • Twitter Clean Grey
  • LinkedIn Clean Grey
bottom of page